Skip to main content

Wabunge wa Chadema waachiwa kwa Dhamana

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro imetupilia mbali hati ya kiapo cha kupinga dhamana ya wabunge Suzan Kiwanga(Mlimba), Peter Lijualikali (Kilombero) na washtakiwa wengine 37 waliofikishwa mahakamani hapo kwa makosa nane.

Mbele ya Hakimu, Ivan Msaki mahakama ilitupilia mbali kiapo hicho na kueleza kuwa washtakiwa wote dhamana yao iko wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili kila mmoja watakaosaini dhamana ya Sh 5 milioni na pia barua za dhamana lazima zisainiwe na wenyeviti wa vijiji ama maofisa watendaji.

Katika kiapo kilichowasilishwa awali mahakamani hapo na upande wa mashtaka kupitia wanasheria wa Serikali, Sunday Hyera na Edga Bantulaki ulieleza sababu walizodai kuwa ni za msingi za kupinga dhamana na kwamba kuwepo nje kwa washtakiwa  kunaweza kuharibu upelelezi wa kesi hiyo.

Kufuatia hoja hiyo upande wa utetezi unaowakilishwa na mawakili wanne wakiongozwa na wakili Peter Kibatala uliamua kuwasilisha hati ya kupinga kiapo hicho kwa madai kuwa  kiliandikwa bila ya kuzingatia misingi na matakwa ya kisheria.

Wakili Kibatala alidai kuwa miongoni mwa mapungufu yaliyokuwemo kwenye kiapo hicho ni pamoja na kutokuonyesha majina ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Malinyi (OCD) ambaye alitajwa kwenye kiapo hicho kama chanzo kilichotoa taarifa zilizotengeneza mashtaka yanayowakabili wabunge hao na wenzao.

Alidai kuwa mapungufu mengine yaliyokuwepo kwenye kiapo hicho ni utofauti wa tarehe ya kuandika kiapo hicho na kusainiwa na hivyo waliiomba mahakama kuzingatia mapungufu hayo.

Kutokana na mvutano huo wa kisheria baina ya pande hizo mbili Hakimu Msaki aliamua kupitia hoja za msingi za kisheria na hivyo kubaini mapungufu yaliyopo kwenye kiapo hicho na kueleza kuwa mapungufu hayo hayawezi kurekebishwa na kwamba kazi ya mahakama ni kutafsiri sheria na si kufundisha namna ya kuandika kiapo.

Kwa msingi huo Hakimu Msaki alitupilia mbali hati hiyo ya kiapo cha kupinga dhamana na kueleza kuwa washtakiwa hao watakuwa nje kwa dhamana wakati kesi yao ikiendelea.

Kabla ya kupewa dhamana washtakiwa hao walikaa rumande kwa siku 12 hali iliyosababisha kesi hiyo kuvuta hisia za watu hususani viongozi na wanachama Chadema waliokuwa wakifulika mahakamani hapo.

Comments

Popular posts

Ugonjwa wasababisha Manji kutofika mahakamani

Mfanyabiashara nchini, Yusuf Manji ameshindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi yake inayomkabili kutokana na kuwa mgonjwa. Kesi hiyo ya uhujumu uchumi imeahirishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutokana na mtuhumiwa huyo kutofika mahakamani hapo. Wakili wa serikali Estazia Wilson ameiambia Mahakama mbele ya Hakimu, Godfrey Mwambapa kuwa Manji hajafika Mahakamani hapo kwa vile ni mgonjwa ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 25 mwaka huu itakapotajwa tena. Manji na watuhumiwa wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka saba yakiwemo ya uhujumu uchumi, kukutwa na mihuri miwili ya JWTZ, ukiwemo wa Mkuu wa Kikosi cha 21 JWTZ, wa Mkuu wa Kikosi Makutupora Dodoma (JWTZ) na wa Commanding Officer Korogwe na magari ya serikali. Watuhumiwa wengine katika sakata hilo ni Deogratius Kasinda na Thobias Pwere na mwingine ambaye jina lake halikufahamika mara moja, wote wamerudishwa rumande.

Mwanzo wa mwisho wa dunia utakuwa Jumatatu 21 Agosti?

Jua litapatwa na mwezi kikamilifu Amerika kaskazini kwa mara ya kwanza kabisa Jumatatu tangu 1918 Mnamo Jumatatu tarehe 21 Agosti, tukio lisilo la kawaida litashuhudiwa Amerika Kaskazini, ambalo limewavutia watu zaidi ya milioni saba wanaotarajia kulishuhudia katika miji mbalimbali Marekani. Kwa mara ya kwanza tangu 1918, jua litapatwa kikamilifu na mwezi Marekani. Bara lote la Amerika Kaskazini litafunikwa na giza totoro mchana. Ingawa baadhi ya watu wanalitazama tu kama tukio la kuvutia, kwa wengine, hili linaashiria mwisho wa dunia kama tunavyoifahamu kwa sasa. Makundi mbalimbali ya Kiinjilisti nchini Marekani kwa mfano, yameanza kuhubiri kwamba tukio hilo linaashiria kukaribia kwa mwisho wa dunia. Tovuti moja ya unabii wa Kikristo kwa jina Unsealed imedai kwamba tukio hilo la Jumatatu litaanzisha kipindi cha Majonzi, kipindi cha miaka saba ambapo katika kipindi hicho asilimia 75 ya watu wote duniani wataangamizwa. Kwa wengine hata hivyo, ni tukio ambalo wamesubiri san...