Mwili wa mtoto Lucia Thomas ambaye amefanyiwa ukatili ukiwa ndani ya Jeneza ukiagwa na kusafirishwa kwenda wilayani Bunda mkoani Mara kwa ajili ya mazishi.
Baadhi ya majirani,ndugu,jamaa na marafiki wakiwa nje kwa ajili ya kuaga mwili wa marehemu.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkoani, Salvatory
Edward akisisitiza kufungwa kwa vituo bubu vya kufundishia wanafunzi
kwenye mtaa ambao anauongoza.
Mchungaji wa Kanisa la Heri wenye moyo safi , Samwel Samson akihubiri na kutoa neno la faraja kwa familia.
Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye hali ya masikitiko na maombolezo. Picha na Joel Maduka,Geita
***
Mtoto Lucia Thomas mwenye umri wa miaka
12 amekutwa akiwa ameuawa na mwili wake kutupwa eneo la makaburi mtaa
wa mkoani mjini Geita.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mkoani, Salvatory
Edward amedai pamoja na kunyongwa hadi kufa, mwili wa mtoto huyo
aliyehitimu darasa la saba mwaka huu katika Shule ya Msingi Kiandege
wilayani Bunda pia ulikuwa na dalili za kubakwa kabla ya kuuawa.
Mama mkubwa wa mtoto huyo Bi, Grace
Thomas amesema hata wao wameshangazwa na tukio hilo kwani mtoto huyo
alikuja Geita akitokea Jijini Mwanza akiwa salama na kwamba kwa mtu
ambaye ametenda ukatili huo ni vyema kwa vyombo vya sheria vikafuatilia
kwa umakini hili waweze kumchukulia hatua za kisheria.
Mama Mzazi wa Mtoto huyo Bi, Mary Thomas
alisema mwanaye alitoka nyumbani juzi Alhamis saa 12:30 jioni akiwa
ameongozana na mtu aliyesema ni mwalimu wake wa masomo ya maandalizi ya
kujiunga na kidato cha kwanza kwa maelezo kuwa anaenda kuchukua karatasi
za mitihani ya somo la Uraia.
Aidha ameongeza kuwa baada ya kuona
usiku umeingia bila mtoto kurejea nyumbani, alikwenda kwa mwalimu
mwingine aliyemtaja kwa jina moja la ambapo waliongoza hadi nyumbani kwa
mwalimu aliyeondoka na mwanaye na kumkuta lakini akawatoroka kwa
kujifanya anampa mtu begi alilolishika mkononi.
Baada ya mwalimu huyo kutorejea huku
mtoto haonekani, waliendelea kumtafuta mtoto wake usiku kucha bila
mafanikio ndipo alipoenda kutoa taarifa polisi alikotakiwa kurejea iwapo
itapita saa 24 bila mtoto kurejea nyumbani.
“Kabla ya saa 24 kumalizika, taarifa
zilinifikia kuwa mwili wa mwanangu umeonekana makaburini akiwa tayari
amefariki huku ukiwa na michubuko shingoni na akiwa amefungwa kamba
miguuni huku hana nguo ya ndani,” alisema Bi,Mary .
Kutokana na tukio hilo, uongozi wa
serikali ya mtaa wa mkoani umepiga marufuku vituo vyote vya masomo ya
ziada eneo hilo na kuwataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao
kwenye shule zinazotambulika kisheria badala ya vituo vya vichochoroni.
Comments