Shahidi wa tano wa Jamhuri katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amedai mahakamani kwamba alipomsikia mtuhumiwa akitamka Rais Dk. John Magufuli ni rais uchwara na ni rais dikteta, alisogea pembeni, hakuendelea kusikiliza.
Shahidi huyo, Timos Emekea (44), alidai hayo jana wakati akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mwambapa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Alidai aliona baadhi ya askari wanasogea kutokana na maneno ya Lissu na akahisi kuna kitu kinaweza kutoka, hivyo akajiondokea na safari zake.
Emekea ambaye ni mkazi wa Goba, alidai siku hiyo ya tukio ya Juni 28, 2016 alikuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akimdhamini mfanyakazi wake saa tano asubuhi.
Alidai akiwa mahakamani hapo, aliona umati wa wananchi, waandishi wa habari na Lissu ambaye huwa anamuona kwenye TV alizungumza maneno ambayo hakupendezwa nayo.
Wakili Peter Kibatala alimuhoji shahidi huyo kwamba Lissu aliyatamka maneno yaliyoandikwa kwenye hati ya mashtaka ama aliyoyaeleza katika ushahidi wake.
Shahidi alidai ni maneno yaliyoandikwa katika hati ya mashtaka na kwamba Serikali iliyotajwa ya kidikteta ni Serikali hii ya Tanzania.
Kibatala alipohoji ni wapi Serikali ya Tanzania imeandikwa kwenye hati ya mashtaka, alijibu hakuna.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 4, 2017.
Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Rais wa TLS na Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anadaiwa kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Anadaiwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alitoa kauli za uchochezi kuwa: “Mamlaka ya Serikali mbovu ni ya kidikteta uchwara, inahitaji kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote, huyu diktekta uchwara lazima apingwe kila sehemu. Kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga, nchi inaingia ndani ya giza nene.’’
Katika kesi hiyo, tayari mashahidi wawili wa upande wa mashtaka, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Kimweli na Staff Sajenti Ndege wamekwishatoa ushahidi wao.
Comments