Skip to main content

Kauli ya Zitto juu ya Ndege ya Tanzania Kuzuiliwa


Picha ya Zitto Kabwe Ruyagwa

Image result for picha ya zitto kabwe

Suala la ndege yetu kuzuiwa nchini Canada lisifanywe ni suala la ushabiki kama ushabiki wa mpira. Ni suala la Nchi hili, na mjadala wake ni lazima uwe na hadhi hiyo. Kitendo cha Kaimu Msemaji wa Serikali kulaumu wanasiasa kwa jambo la kisheria kama hili ni utoto. Historia yetu inaonyesha hakuna mwanasiasa (hasa wa upinzani) anayeweza kushirikiana na kampuni za kigeni kuhujumu nchi.
Falsafa ya chama ninachokiongoza, ACT Wazalendo, ni 'Taifa Kwanza, Leo na Kesho'. Mimi binafsi filosofia yangu ni rahisi sana 'My Country First, Right or Wrong' (Nchi Yangu Kwanza, Kwa Usahihi au Kwa Makosa). Maneno yanayosambazwa kuwa nimeshiriki kuwezesha ndege ya Bombardier iliyonunuliwa na Serikali Kwa niaba ya ATCL kukamatwa huko Canada ni takataka tu zinazosambazwa na wapika propaganda. Ni upuuzi!
Serikali lazima ifahamu kuwa ni lazima ihojiwe, na iwe tayari kutoa majibu. Sisi kama vyama vilivyo Nje ya Serikali ni wajibu wetu kuhoji jambo lolote. Pia ni haki yetu kupata Taarifa zozote kutoka mahala popote zitakazosaidia kuisimamia Serikali. Wajibu wa Serikali ni kujibu hoja zinazoibuliwa nasi. Majibu ya Msemaji wa Serikali yanataka kuligeuza suala hili kuwa la kisiasa na watu wameangukia kwenye ushabiki huo.
Tusikubali kuingia kwenye huu ushabiki. Hili ni suala la kisheria, na ni suala la nchi ambayo sisi wote tuna maslahi ya kuona inakwenda mbele.
Nchi yetu kudaiwa sio dhambi. Hata mataifa makubwa duniani yanadaiwa. Watu binafsi tunadaiwa sembuse Serikali? Mimi binafsi ninadaiwa madeni ya uchaguzi mpaka sasa, na wengine (kati ya wanaonidai) wamenipeleka mahakamani. Sio dhambi kudaiwa.
Muhimu ni (1) Je Deni limetokana na Nini? Ni maamuzi mabovu ya kisiasa? (2) Unalipa deni hilo au kuweka mikakati ya kulipa?
Serikali yetu inafahamu kuwa nchi yetu ina madeni mengi, na miongoni mwa madeni hayo yapo ambayo yameshaamuliwa na Mahakama. Kinachopaswa ni kuwa na MAARIFA ya kupita ili kuzuia Mali zetu nje ya nchi kuzuiwa kama ilivyo Kwa Ndege hii.
Serikali iwe wazi kuhusu suala hili la Ndege. Je ile ya Boeing (Terrible Teen) ipo salama? Madeni mengine yenye amri ya mahakama ni yepi? Kwanini Serikali inasubiri kuhojiwa ndipo itoe Taarifa?
Hii ni nchi yetu sote. Hakuna mwenye hatimiliki ya ukweli. Ukweli pia haupendi kupindwapindwa. Serikali itoke kueleza nini kimetokea mpaka Ndege kuzuiwa, iachane na tabia ya hovyo ya kutafuta mchawi 'kwamba eti wanasiasa ndio wamesababisha'. Kutafuta mchawi ni kutowajibika kwa maamuzi ya Serikali yenyewe.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama - ACT Wazalendo
Jimboni Kigoma Mjini
Agosti 20, 2017

Comments

Popular posts

Ugonjwa wasababisha Manji kutofika mahakamani

Mfanyabiashara nchini, Yusuf Manji ameshindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi yake inayomkabili kutokana na kuwa mgonjwa. Kesi hiyo ya uhujumu uchumi imeahirishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutokana na mtuhumiwa huyo kutofika mahakamani hapo. Wakili wa serikali Estazia Wilson ameiambia Mahakama mbele ya Hakimu, Godfrey Mwambapa kuwa Manji hajafika Mahakamani hapo kwa vile ni mgonjwa ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 25 mwaka huu itakapotajwa tena. Manji na watuhumiwa wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka saba yakiwemo ya uhujumu uchumi, kukutwa na mihuri miwili ya JWTZ, ukiwemo wa Mkuu wa Kikosi cha 21 JWTZ, wa Mkuu wa Kikosi Makutupora Dodoma (JWTZ) na wa Commanding Officer Korogwe na magari ya serikali. Watuhumiwa wengine katika sakata hilo ni Deogratius Kasinda na Thobias Pwere na mwingine ambaye jina lake halikufahamika mara moja, wote wamerudishwa rumande.

Mwanzo wa mwisho wa dunia utakuwa Jumatatu 21 Agosti?

Jua litapatwa na mwezi kikamilifu Amerika kaskazini kwa mara ya kwanza kabisa Jumatatu tangu 1918 Mnamo Jumatatu tarehe 21 Agosti, tukio lisilo la kawaida litashuhudiwa Amerika Kaskazini, ambalo limewavutia watu zaidi ya milioni saba wanaotarajia kulishuhudia katika miji mbalimbali Marekani. Kwa mara ya kwanza tangu 1918, jua litapatwa kikamilifu na mwezi Marekani. Bara lote la Amerika Kaskazini litafunikwa na giza totoro mchana. Ingawa baadhi ya watu wanalitazama tu kama tukio la kuvutia, kwa wengine, hili linaashiria mwisho wa dunia kama tunavyoifahamu kwa sasa. Makundi mbalimbali ya Kiinjilisti nchini Marekani kwa mfano, yameanza kuhubiri kwamba tukio hilo linaashiria kukaribia kwa mwisho wa dunia. Tovuti moja ya unabii wa Kikristo kwa jina Unsealed imedai kwamba tukio hilo la Jumatatu litaanzisha kipindi cha Majonzi, kipindi cha miaka saba ambapo katika kipindi hicho asilimia 75 ya watu wote duniani wataangamizwa. Kwa wengine hata hivyo, ni tukio ambalo wamesubiri san...