WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wamevamia Msikiti Mkuu wa Ijumaa ulioko Kata ya Igunga Mjini wilayani hapa mkoani Tabora, kisha kumjeruhi mlinzi na kupora baadhi ya vitu ikiwemo vitabu vya dini ya Kiislamu. Mlinzi aliyejeruhiwa ni Juma Mussa (55), mkazi wa Mtaa wa Nkokoto kata ya Igunga ambaye amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga na hali yake bado ni mbaya. Mkuu wa Wilaya ya Igunga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, John Mwaipopo alithibitisha kutokea kwa uhalifu huo na mtuhumiwa mmoja amekamatwa pamoja na vitu vilivyoibwa. Alimtaja mtuhumia huyo kuwa ni Juma Mponi (45) ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Stendi ya Mabasi mjini Igunga, na kutamba kuwa hakuna jambazi atakayetoka salama Igunga kwa kuwa polisi wamejipanga kikamilifu kukabiliana na matukio kama hayo. Akizungumza kwa shida akiwa wodini, mlinzi huyo alisema shambulio hilo limetokea Septemba 25, ...